BILLIONI 21 ZATENGWA KUTATUA TATIZO LA VITABU SEKONDARI

RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali imetenga Sh bilioni 21 katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/2015 kwa ajili ya kumaliza tatizo la upungufu wa vitabu kwenye shule za sekondari.

Kauli hiyo ameitoa wakati akihutubia wananchi wa kata ya Kimbe baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye maabara ya masomo ya sayansi ya sekondari ya kata hiyo ambapo ujenzi wake utagharimu jumla ya Sh milioni 135 hadi kukamilika.
Mpaka sasa ujenzi wa maabara hiyo ya masomo ya fizikia, kemia na baolojia ulioanza mwaka jana umegharimu Sh milioni 59 . Kati ya hizo mchango wa wananchi ni Sh milioni 47.4, halmashauri Sh milioni 12.5 na kiasi kilichobaki ni mchango wa serikali kuu.
Ujenzi utakamilika Novemba mwaka huu. Rais alisema fedha hizo zimeongezwa ili kukabiliana na uhaba wa vitabu vikiwemo vya masomo ya baolojia, kemia, fizikia na hisabati ili kuwawezesha wanafunzi wanaosoma katika shule za sekondari hususan za Kata kujifunza masomo ya sayansi.
“Katika mwaka ujao wa fedha tumeamua kuongeza fedha tunazotenga kwa ajili ya ununuzi wa vitabu na lengo hasa la serikali ni kupunguza tatizo lililopo sasa pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia”, alisema.
Aliongeza, “lengo la kuhakikisha msisitizo katika kuboresha mazingira ya utoaji elimu, hasa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi ni kuwezesha kata kupata wataalamu wenye ujuzi katika fani za sayansi ikiwemo Afya, Uhandisi, Madaktari ambao watasaidia kuchochea maendeleo ya jamii husika na taifa kwa ujumla”, alisema.
Aidha, alisema serikali inatambua tatizo la uhaba wa nyumba za walimu na kwamba tayari imetenga Sh milioni 500 kwa kila halmashauri nchini kupunguza tatizo hilo.
“Kwa kutambua umuhimu wa shule za sekondari za kata serikali imeamua kutenga Sh milioni 500 kwa kila halmashauri kuendeleza mpango wa ujenzi wa nyumba za walimu ambao utaboresha mazingira yao ya kazi na kuongeza uhakika wa walimu shuleni”.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Daudi Mayeji akizungumzia utekelezaji wa Mpango wa dharura wa serikali wa kukabiliana na uhaba wa maabara alisema kwa Kilindi tayari halmashauri imenunua maabara nne zinazotembea zenye thamani ya Sh milioni 10 mwaka huu wa fedha.
Awali Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo alimweleza rais kuwa tatizo kubwa linalowakabili wananchi wake ni bei ndogo ya mazao hasa mahindi ambapo wakati wa msimu wa mavuno debe moja linauzwa kwa Sh 2,400.
Akijibu ombi hilo rais alisema atawaelekeza wakala wa taifa wa ununuzi wa mazao wenye ofisi zao wilayani Handeni (NFRA) kununua mahindi ya wakulima wa wilayani Kilindi ili kuwawezesha kujikwamua ki uchumi.