
Apinga mawaziri kushambuliwa hadharani
KATIBU Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, amekosoa mwenendo wa chama chake na kueleza kuwa kwa namna kinavyoendeshwa kinajipa wakati mgumu. (HM)
Makamba alisema kitendo cha viongozi
wa chama hicho kuwataja hadharani baadhi ya mawaziri kwamba ni mizigo,
si kizuri kwa maslahi ya chama hicho.
Makamba alifanya mahojiano maalumu na
gazeti hili nyumbani kwake Wazo Tegeta, nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia nafasi ya CCM
kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumzia hoja hiyo, Makamba
alisema hatua ya chama hicho kuwataja hadharani baadhi ya mawaziri
wasiowajibika ni kuvipa ajenda vyama vya upinzani na kwamba hiyo ni sawa
na kujimaliza mbele ya wananchi.
Kauli ya Makamba inaonekana wazi
kumpinga Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ambao hivi karibuni walitaja hadharani
majina ya mawaziri watatu kwamba ni mizigo.
Wakiwa katika ziara za kichama katika
mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Songea, Kinana na Nape waliwashukia mawaziri
hao ambao ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza
na Naibu wake, Adamu Malima.
Wengine waliotajwa na viongozi hao ni
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, kwamba kwa
pamoja wameshindwa kutatua matatizo ya wananchi.
Makamba alisema, CCM itajijengea
heshima iwapo itaendelea kuwa na utaratibu wa kutumia vikao vya chama
kuwashughulikia mawaziri wasiotimiza wajibu wao badala ya kuwaumbua
hadharani.
Kwa mujibu wa Makamba, hatua ya
kuwaita mawaziri mizigo hadharani ilikuwa ni sawa na kujiumbua wenyewe
na kukivunjia heshima chama hicho.
"Ndio maana chama kina vikao, kama
waziri ni mzigo mwiteni katika vikao, kumsema hadharani ndio sipendi
hata kidogo na tusemane kwenye vikao na si mahala pengine.
"Kumsema mwenzako hadharani siyo
vizuri yule ana mke, anao watoto, anao ndugu zake, hawa wote hawapendi
na hawataki, sifurahishwi kuwapigia kelele hadharani mnajiumbua wenyewe.
Lazima tukijengee heshima chama.
"Haya ya kusemana hadharani si mazuri,
chama kinakwenda kwenye uchaguzi 2015 mtawaeleza nini wananchi, hamuoni
kwamba mtaonekana hamfanyi kazi?" Alihoji Makamba.
Katika mazungumzo hayo, Makamba
aligusia uhusiano wake wa kikazi na baadhi ya wenzake katika chama na
kusema mara nyingi alikuwa akisumbuliwa kutokana na kusema ukweli.
Bila kufafanua Makamba kwa sauti ya
chini na ya huzuni, alisema ukweli umekuwa ukimsumbua kati yake na
wenzake lakini amekuwa akiweka ushahidi kwa kila analolitamka au
kulitenda.
"Nimekuwa nikipata shida kutokana na
kusema ukweli. Ukweli unanisumbua sana kwa wenzangu, lakini inanibidi
nikisema niweke ushahidi," alisema Makamba bila kufafanua.
Makamba alisema CCM inaendelea kufanya
kazi kubwa na nzuri ndani ya chama. "Kazi ya chama ndani ya chama ni
vikao, wanachama kukutana na kushiriki katika vikao na viongozi pamoja
na kulipa ada.
"Mimi ni mwanachama wa Tawi la Tegeta Kisanga, naalikwa katika vikao vya chama na vijana, hivi vinafanyika.
"Kazi ya chama ndani ya umma ndio hizi
kazi zinazofanyika kujenga shule za msingi na sekondari, kupeleka maji
kwa wananchi, barabara na uchukuzi na sisi ndio chama tawala tuliahidi
katika manifesto," alisema Makamba.
Ziara za akina Kinana
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahaman Kinana aliripotiwa akiwa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya
akisema kuwa CCM imepoteza imani kwa wananchi kutokana na kukorogana kwa
viongozi wenyewe kwa wenyewe.
Katika kikao na wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM, Wilaya ya Rungwe, Kinana alisema CCM itachukua hatua za
kuwawajibisha viongozi wakiwamo wa Serikali walioshindwa kuwajibika.
Akiwa Songea, Kinana alinukuliwa
akimtaja hata aliyekuwa Waziri wa Fedha marehemu, Dk. William Mgimwa
kuwa ni miongoni mwa mawaziri 'mizigo' na kuahidi kuwashughulikia katika
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akiwa Namtumbo mkoani Ruvuma, Kinana
aliwataja Chizza na Malima kuwa tangu wateuliwe wameshindwa kutekeleza
wajibu wao wa kuongoza wizara hiyo na hakuna hata siku moja waliyofika
Ruvuma kushughulikia matatizo ya wakulima wa mazao ya tumbaku, mahindi
na mpunga.
Nape pia alinukuliwa akimtaja, Dk.
Shukuru Kawambwa akisema kuwa licha ya kushindwa kuongoza Wizara ya
Elimu, lakini pia anatakiwa kuchukuliwa hatua kutokana na mkataba
alioingia na wakandarasi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Namtumbo hadi
Tunduru mkoani Ruvuma.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa
CCM, Philip Mangula, amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akikemea
tabia ya baadhi ya viongozi serikalini kutowajibika.
Mbali na suala hilo, Mangula pia hivi
karibuni alikemea tabia ya baadhi ya wanachama wa chama hicho ambao
wameanza kutangaza nia ya kuwania nafasi mbalimbali ikiwamo urais,
ubunge na udiwani kabla ya muda.
"Kuna baadhi ya wanachama wetu
wanapita mitaani na kujifanya wanatoa misaada kama vile wafadhili, huku
wakitangaza nia ya kuwania uongozi, hao ni waasi chama hakitawavumilia,"
alinukuliwa Mangula. Chanzo: mtanzania _and Mjengwa blog