![]() |
Gari
aina ya Lori Fuso lenye namba za usajili T. 284 AGL ambalo lilikuwa na
shehena aina ya mirungi viroba vipatavyo 173 vyenye jumla ya uzito wa
kilogramu 1800
![]() |
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus
Sabas akiongea na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya jinai Mkoa wa Arusha
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Camirius Wambura aliyeshika madawa ya
kulevya aina ya mirungi nje ya jengo la Makao Makuu ya jeshi hilo
mkoani hapa mara baada ya kukamata shehena hiyo.(Picha na Rashid Nchimbi
wa Polisi Arusha)
…………………………………………………
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wiki moja tu baada ya jeshi la Polisi Mkoani Arusha kukamata lori aina
ya Mitsubishi Canter lililokuwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi,
leo tena Jeshi hilo limekamata shehena nyingine ya madawa ya aina hiyo
ambayo ilikuwa kwenye lori aina ya Fuso lenye namna za usajili T. 284
AGL
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa
Polisi (ACP) Liberatus Sabas alisema kwamba tukio hilo limetokea leo
muda wa saa 12:30 asubuhi eneo la Engarenaibo lililopo wilayani Longido
ambapo madawa hayo yalikuwa yanasafirishwa kutoka nchi jirani ya Kenya
kuja hapa nchini kupitia mpaka wa Namanga.
Aliongeza kwa kusema kwamba mirungi iliyokamatwa ni jumla ya viroba 173
vyenye uzito wa kilogramu 1800 na mafanikio hayo yalipatikana baada ya
jeshi hilo kupata taarifa toka kwa raia wema na mtu mmoja alikamatwa na
anaendelea kuhojiwa huku mwingine akifanikiwa kukimbia.
Baadhi ya viroba hivyo vilionekana kuwa na majina ya watu, uzito na
mahali, hali inayotafsiriwa kuwa huwa vinagawanywa kwa watu hao mara
baada ya kuingizwa mjini hapa.
Kamanda Sabas aliendelea kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu kwa
ushirikiano wao mkubwa na kuwaomba waendelee kushirikiana na jeshi hilo
hali ambayo itasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu.
Pia Kamanda Sabas aliwaonya wamiliki wa vyombo vya usafiri hasa magari
kutokubali vyombo vyao vitumike katika usafirishaji wa biashara haramu
kwani pindi vinapokamatwa huwa vinakuwa chini ya vyombo vya dola huku
kesi ikiendelea badala ya kuendelea kufanya kazi nyingine za uzalishaji.
Mpaka hivi sasa kwa muda wa wiki moja ndani ya mwezi huu jumla ya
magari mawili yamekamatwa.

